Uongozi wa kijiji cha
Fella Walalamikiwa
Na Antony Sollo Mwanza
August 01 2014.
UONGOZI
wa kijiji cha Fella Wilayani Misungwi Mkoani Mwanza unalalamikiwa kuuza shamba
la Bernadeta Valentine lenye ukubwa
ekari 15 kwa mwekezaji wa kichina kwa shilingi milioni sitini 60,000,000.
Wanaolalamikiwa kuuza shamba hilo ni Kaimu Mwenyekiti wa
kijiji cha Ngeleka Donald Mongo akishirikiana na Halmashauri ya kijiji hicho
pamoja na Afisa Mtendaji wa Kata ya Fella ambaye pia ni Kaimu Afisa Mtendaji wa
Kijiji cha Ngeleka Thomas Shunashu.
Akizungumza na Tanzania Daima Bernadeta alisema kuwa,njama zote za kuchukua eneo lake
hilo zilifanywa na viongozi wa baraza la Ardhi la Kata ya Usagara enzi hizo
wakati wa kusikiliza shauri lake namba
17/2010 kipindi cha 2009/2012 lililokuwa likiongozwa na Mwenyekiti aliyestaafu
Nestory Majige.
Bernadeta alidai
kuwa kulikuwa na njama za maksudi zilizofanywa na viongozi wa baraza hilo kwa kumnyima hukumu yake,ili kufanikisha
mpango wa kupora shamba na kuliuza kama ilivyofanyika sasa.
Tanzania Daima lilifanikiwa kupata nakala ya barua yenye
kumbukumbu namb FELLA/MDC/5.01/010 ya 22/10/2010 iliyokuwa ikimjibu Bernadeta
kuwa hana haki na shamba hilo majibu ambayo hakuridhika nayo.
Bernadeta alilalamikia kitendo cha baraza la Kata ya Usagara
kukaa zaidi ya miaka miwili bila kumpa nakala yake ya hukumu ili aweze kukata
rufaa ambapo alipeleka malalamiko yake ya kutopatiwa nakala ya hukumu kwa Afisa
Tarafa ya Usagara Perpetua Chonja.
Afisa Tarafa Chonja alimwita Afisa Mtendaji wa Kata ya Fella
kwa barua yenye kumb namb KTU/CS.20/19/13 ya tarehe 25/09/2013 hii ikiwa ni
jitihada za kusaidia kutatua mgogoro huo bila mafanikio.
Wakati akitafuta msaada sehemu mbalimbali Bernadeta
alisikia kuwa shamba lake limegawiwa kitongoji cha Ngeleka na mali zote
zimekuwa ni za kijiji cha Ngeleka bila hata kushirikishwa huku viongozi wa
kijiji hicho wakiuza kipande cha shamba hilo kwa Wakala wa Barabara Tanroads na hivyo Bernadeta alirudi tena kwa Afisa Tarafa
ili asaidiwe kupata msaada juu ya kuuzwa kwa shamba lake na kutopatiwa nakala
ya hukumu yake Mwenyekiti wa baraza hilo Nestory Majige.
Imedaiwa kuwa Chonja alitoa maelekezo kwa
baraza hilo ambapo Baada ya viongozi wa baraza hilo kupokea maelekezo hayo
Mwenyekiti wa Baraza hilo Nestory Majige alimpatia Bernadeta hukumu ambayo
haikusainiwa na wajumbe wa baraza pamoja
na Mwenyekiti wa baraza hilo.
Tanzania Daima lilimtafuta Afisa Mtendaji wa
Kata ya Fella ambaye pia ni Kaimu Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Fella Thomas
Shunashu kujibu tuhuma zilizoelekezwa kwake na viongozi wa Kijiji cha Fella
ambapo Shunashu alikiri kusikia jambo hilo lakini akadai kuwa hakuwahi kuonana
na Bernadeta kiofisi.
“Ndugu Mwandishi mimi sina tatizo na huyu
mama niko tayari kukutana naye ili niweze kumsikiliza na kumsaidia lakini nasikia
maneno mengi mno mitaani mimi yananiumiza moyoni na ninaogopa kukutana naye
tukiwa wawili kwa kuwa nahofia usalama wangu.”
Kuhusu kuuzwa kwa shamba hilo Shunashu
alisema kuwa yeye hahusiki na jambo lolote ila maamuzi ya kuuzwa kwa shamba
hilo ni ya Halmashauri ya Kijiji cha Ngeleka ambao waliamua kuuza mali za
Kijiji kwa ajili ya Maendeleo yaKijiji chao.
“ ni
kweli shamba hilo limeuzwa kwa mwekezaji jumla ya shilingi milioni sitini 60,000,000
ambazo ziko katika Akaunti ya Kijiji cha Ngeleka huku akikana kujinufaisha kwa
namna yoyote ile na kuuzwa kwa shamba hilo.
Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi la Kata ya
Usagara kipindi cha 2009/2012 alipotafutwa kujibu tuhuma hizo alitoa kauli ya
kejeli “huyu mama ni mwendawazimu na
ningejua kuwa ulikuwa unanitafuta kwa ajili ya kuzungumzia suala hili
nisingekuja”.
Tanzania Daima liliwatafuta wajumbe wa
halmashauri ya Serikali ya Kijiji cha Ngeleka kuzungumzia tuhuma hizo wao
walikataa kuzungumza lolote na kusema kuwa wanaoweza kulizungumza suala hili ni Afisa Mtendaji Thomas Shunashu kwa madai
kwamba ndiye aliyeratibu zoezi hili.
Afisa Ardhi wa Wilaya ya Misungwi Fredy Nyoka
alikiri kupokea malalamiko ya Bernadeta na kusema kuwa anazo taarifa suala hilo
kuwa lilipelekwa katika Mahakama zinazohusika na thamani ya madaiya mlalamikaji.
Nyoka alidai pia kupata taarifa za Afisa
Mtendaji wa Kata ya Fella Thomas Shunashu kufanya taratibu za uuzaji wa mali za
Kijiji hicho kinyemela na kumuonya kuwa mambo haya yanaweza kumletea matatizo.
“Afisa Mtendaji huyo alikuwa akifanya mambo
haya bila kutushirikisha sasa siku moja alitaka kuhamisha fedha zilizoingizwa
katika Akaunti ya Serkali ya Kijiji shilingi milioni sitini 60,000,000 akazuiwa
na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi Nathan Mshana akiambiwa kuwa
fedha yoyote ikiingia kwenye Akaunti ya serikali ya Kijiji mwenye mamlaka na
uhamishaji wa fedha hizo ni Mkurugenzi pekee ambapo mpangowa kuhamisha fedha
hizo uligonga mwamba alisema Nyoka.”
Mwisho
0 comments:
Post a Comment