MNEC
Misungwi aitaka TANROADS kutoa Elimu
Na
Antony Sollo Mwanza.
26JUNE 2014
MJUMBE wa mkutano Mkuu wa chama cha Mapinduzi Jackob Dalali
Shibiliti amewataka wakala wa Barabara Nchini TANROADS Mkoa wa Mwanza kufika
katika kijiji cha Misasi Wilayani Misungwi kuzungumza na wananchi kuhusu
operesheni ya bomoabomoa ya nyumba zilizo ndani ya hifadhi ya barabara.
Akizungumza na Tanzania Daima,Shibiliti alisema kuwa wakala
wa barabara Mkoa wa Mwanza,walipita wakitangaza juu ya Operesheni hiyo ambayo
itafanyika kupisha ujenzi wa barabara ya Mwanangwa Salawi lakini akishangazwa
na uamzi usio shirikishi kwa wananchi kwa kuwa,hakuna mkutano wowote uliowakutanisha
wadau na kujadili faida za ujenzi wa barabara hiyo.
Katika ufuatiliaji wake Mjumbe huyo wa NEC alikutana na
watendaji wa TANROADS Mkoa wa Mwanza na kufanya mazungumzo ya kina huku
akiwaomba wafike katika vijiji vinavyopitiwa na mradi huo kwa ajili ya kutoa
Elimu kwa wananchi hao.
Shibiliti amevitaja vijiji vitakavyopitiwa na mradi huo
kuwa ni Mwawile,Misasi ,Kijima Busongo, kabala, Mwagiligili naInonelwa na
kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kupatiwa elimu hiyo ili
kuweza kujua faida na hasara ya mradi huo.
Wakitoa maoni yao baadhi ya wazee wa maeneo ya Misasi
akiwemo Msafiri Mchenya wameishauri Tanroads kuangalia uwezekano wa kuipitishia
barabara pembeni mwa mji kwa ajili ya kuondoa usumbufu kwa wananchi na pia
kuepuka matumizi mabaya ya fedha za umma kwa,kuwa hakukuwepo taarifa na elimu juu
ya hifadhi ya barabara tangu mwanzo hivyo kuonekana kuwa jambo hili sasa ni
jipya.
Tanzania Daima lilifika Ofisi za wakala wa barabara kujua
hatma ya mchakato huo na kukutana na Mhandisi wa Barabara kuu Mkoa wa Mwanza
Pius Joseph ambaye alikanusha madai hayo na kusema kuwa lengo lililowapeleka
huko ni kutoa elimu juu ya sheria mpya ya hifadhi ya barabara na 13 ya mwaka
2007 (Road Act No 13 of 2007).
Pius alisema kuwa,kwa mujibu wa kanuni ya 29 (1)a na b ya
mwaka 2009 ya sheria hii eneo la hifadhi ya barabara limeongezeka na kuwa mita
60 (sitini) yaani mita 30 kuanzia katikati ya barabara kila upande kwa barabara
zote kuu na Mkoa.
Mhandisi Joseph aliendelea kufafanua kuwa hapo awali eneo
la barabara lilikuwa ni mita 45 yaani mita 22.5 kila upande wa barabara na
kusema kuwa kuanzia sasa wananchi wafahamu kuwa ni kosa kwa mujibu wa sheria
kujenga nyumba,kufyatua matofali,kulima au kufanya shughuli yoyote ndani ya
mita 60 (sitini) yaani mita 30 kila upande wa barabara.
Tanzania Daima linayo nakala ya maelekezo ya Meneja wa
wakala wa barabara Mkoa yenye kumb Na TNRD/RM/MZA/B.1570/VI/40 ikifafanua juu
ya kwenda kwa wataalamu hao wilayani misungwi kwa lengo la kutoa elimu na si
kwenda kutoa taarifa ya kuvunjwa kwa nyumba za wananchi wilayani humo.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi Nathan
Mshana alipotafutwa kuzungumzia suala hilo simu yake iliita bila kupokelewa na
juhudi za kumtafuta zinaendelea.
Mwisho.
0 comments:
Post a Comment