Wednesday, October 26, 2016

Mtendaji Amchongea Mkurugenzi kwa DC





Na Antony Sollo Misungwi.

AFISA Mtendaji wa Kijiji cha Sanjo Charles Bulugu,amemchongea kwa Mkuu wa Wilaya ya Misungwi Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Eliud Mwaiteleke baada ya kutoa taarifa za uongo katika mkutano wa Serikali ya Kijiji cha Sanjo uliofanyika August 18 mwaka huu akisema  kuwa,Mkurugenzi huyo ameshindwa kufika kijijini hapo kwa kukosa gari la kumpeleka kusikiliza kero za wananchi hao.

Ilidaiwa kuwa Mkuu huyo wa Wilaya alitoa agizo hilo kufuatia malalamiko yaliyotolewa na wananchi wa Kijiji cha Sanjo kuomba Uongozi wa Wilaya ya Misungwi ufike hapo kwa ajiri ya kusikiliza kero zao.
Akitoa taarifa hizo Bulugu alisema kuwa Mkurugenzi amekwama kufika katika mkutano huo kutokana na kukosa usafiri kufuatia gari lake kuwepo katika usimamizi wa mitihani ya Taifa kwa wanafunzi wa Darasa la Saba.
“Ndugu zangu wananchi kwa niaba ya Mkurugenzi  napenda kuwaomba radhi kwa kuchelewa kufika hapa mgeni wetu sasa ni saa tano asubuhi ,ni kwamba mgeni wetu hataweza kufika kutokana na kukosa usafiri wa kumleta hapa,gari lake liko kwenye shughuli za Mitihani ya Darasa la saba”alisema Bulugu huku miguno na maswali toka kwa wananchi vikitawala

“Hivi Mtendaji huoni kuwa huu ni uzembe wa makusudi,magari yote ya Halmashauri hayapo kweli? hata gari lake liko kwenye mitihani?mbona hawa watu wanataka kuturudisha tulikotoka? Sasa tunakuagiza Mtendaji ukamwambie Mkuu wa Wilaya kuwa agizo lake limepuuzwa! kwa nini Mkurugenzi asije hata na Hiece?” alihoji mmoja wa wananchi waliokuwepo katika mkuitano huo.

Uchunguzi uliofanywa na MwanaHALISI umebaini kuwa, taarifa hizo hazikuwa za kweli kwani Mkurugenzi huyo alikuwa safari ya kikazi Mjini Dodoma.

Baada ya taarifa hiyo wananchi walionyesha kukasirishwa na kitendo hicho na kuahidi kugomea mikutano ijayo iwapo hawatapata maelezo ya kutosha juu ya tukio hilo.
MwanaHALISI lilimtafuta Mkurugenzi huyo ili kutolea ufafanuzi wa taarifa iliyotolewa na Afisa Mtendaji huyo ambapo Mwaiteleke alisema kuwa habari hizo si za kweli
“Mimi kwa sasa niko Mbeya,nimeshtushwa sana na taarifa hizo mimi nikose usafiri si ningeenda na pikipiki? Sisi kazi yetu ni moja tu nayo ni kuwatumikia wananchi na si vinginevyo sijui Mtendaji huyo kapata wapi maelekezo hayo ngoja nifuatilie”alisema Mwaiteleke.

Wakizungumza na MwanaHALISI kwa nyakati tofauti wananchi hao walisema kuwa wamekwazwa na kitendo cha Mkurugenzi kushindwa kufika kijijini jambo walilosema bila kumung’unya maneno kwamba ni uzembe.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Nyasubi Meni Lutandula ameliambia MwanaHALISI  kuwa kuna udanganyifu mkubwa katika ujenzi wa tenki la maji katika kijiji cha Sanjo ambapo walibaini matumizi mabaya ya fedha za wananchi kiasi cha shilingi 20,828,502;60 katika ujenzi wa mradi wa maji.
 “Inasikitisha kuna ujenzi wa shule lakini nayo haijaanza kufanya kazi lakini tayari vyumba vimechakaa na tayari sisi wananchi tumeshaambiwa kuchangia shilingi 6500 kila familia kwa ajiri ya ukarabati wa vyumba hivyo”.alisema Lutandula.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Sanjo Bukali John alipotakiwa kutolea ufafanuzi sakata la ujenzi wa madarasa hayo kujengwa chini ya kiwango alisema kuwa si vizuri kufuatilia jambo hilo kwa kuwa wananchi tayari wameshakubali kuchangia fedha kwa ajiri ya kurekebisha vyumba hivyo.

“ Ndugu mwandishi ni kweli kuna mapungufu yaliyojitokeza katika ujenzi wa vyumba hivyo lakini nashauri usifuatilie suala hilo maana tayari tumeshafanya vikao na wananchi na kukubaliana kuchangia fedha kiasi cha shilingi 6500 ili tukarabati vyumba hivyo” alisema Bukali.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Misungwi Juma Sweda alisema kuwa hana taarifa zozote juu ya agizo hilo na kwamba yeye hajawahi kufanya ziara katika kijiji cha Sanjo
“Mimi sijawahi kufanya ziara yoyote katika kijiji hicho isipokuwa nilishiriki kikao cha Kamati ya Maendeleo ya Kata ya Fela hivyo sijui Afisa Mtendaji huyo alitoa wapi maelekezo hayo nitafuatilia kujua zaidi juu ya jambo hilo”alisema Sweda.

MWISHO

0 comments:

Post a Comment