CHADEMA
YANASA SIRI NZITO
DC Muleba adaiwa kushiriki utapeli.
Kigogo CCM ajichukulia heka 8000.
Na Antony Sollo Muleba.
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo( CHADEMA) Wilayani Muleba
Mkoani Kagera,kimemtuhumu Mkuu wa Wilaya hiyo,Limbres Kipuyo na baadhi
ya viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilayani humo, kujihusisha
na utapeli wa ardhi ya wananchi.
Tuhuma hizo dhidi ya DC wa Muleba, zilitolewa na
Diwani wa Kata ya Kasharunga, Khalid Hussein, kuwa anajihusisha na genge
linalodaiwa kufanya utapeli katika ofisi mbalimbali kwa ajili ya kujinufaisha
katika eneo linalodaiwa kumilikiwa na kada wa CCM katika kijiji cha
Kiteme .
Akizungumza katika Mkutano wa hadhara uliondaliwa
na Mbunge wa Viti Maalum wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)
Conchesta Rwamulaza ambaye pia ni Katibu wa chama hicho Mkoa wa Kagera,diwani
huyo aliwaeleza wananchi kuwa chama hicho kina dhamira ya dhati ya kuwatumikia
wananchi na kuwaondolea kero na matatizo yao bila kujali itikadi za
vyama na dini zao.
Hussein alisema kuwa mgogoro wa ardhi unaofukuta
katika kitongoji cha Byantanzi katika kijiji cha Kiteme umesababishwa
na baadhi ya makada wa CCM ambao wamejitwalia ardhi ya wananchi ekari
8000 bila kufuata taratibu.
Diwani huyo alisema baada ya kufuatilia alibaini
utapeli huo unaofanywa na viongozi waandamizi wa Serikali na wa CCM
wilayani Muleba, baada ya kunasa barua aliyoandikiwa DC huyo kuhusiana
na utapeli huo.
Katika hali ambayo alidai kuwa inathibitisha kuhusika
kwa Mkuu huyo wa Wilaya kushiriki kwenye sakata hilo ni kutokana na
tamko linaloashiria utekelezaji wa mpango wa utapeli huo kwa kuwaamuru
wananchi kuondoka katika maeneo hayo ifikapo tarehe 15 februari 2014,
huku wakiwa wamelima mazao yao ya aina mbalimbali yanayotarajiwa kukomaa
siku zijazo.
Alidai kuwa marehemu Edward Barongo akiwa Mkuu wa
mkoa wa Kagera wakati huo, alijipatia ardhi yenye ukubwa wa ekari 8000
zaidi ya alizoomba,lakini viongozi wa serikali na chama wakamkingia
kifua,akajipatia ardhi hiyo kinyume cha taratibu.
Wakati DC huyo watuhumiwa,wengine ni viongozi wa
CCM na serikali Wilayani Muleba wanatuhumiwa kujihusisha kumkingia kifua
kada wa CCM Edward Barongo ambaye aliwahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera
katika sakata hilo la kujipatia ardhi yenye ukubwa wa ekari 8000 zaidi
ya hekari alizoziomba ilidaiwa kwenye mkutano huo na Diwani huyo kuwa,
marehemu Barongo aliomba kupatiwa ekari 2000, uombaji ambao hukufuata
kanuni na taratibu, hata ushirikishwaji wa wananchi haukuzingatiwa,hivyo
kuzua mgogoro mkubwa kati ya familia ya marehemu Edward Barongo na wanakijiji
wa Kiteme.
Naye Mbunge wa Viti Maalum wa CHADEMA Conchesta Rwamlaza, akizungumza
alisema kuwa kufuatia kushamiri kwa migogoro ya ardhi nchini,serikali
iwe makini na kuchukua hatua za haraka kutatua migogoro hiyo na akailaumu CCM na serikali yake.
“Serikali ya CCM imeshindwa kuwajali wananchi kaya
zaidi ya 400 watakaoathirika na zoezi la kuondolewa katika maeneo yao.
Haya ndiyo matokeo yakushamiri kwa migogoro hii ya
ardhi kwa wakubwa kupora ardhi ya wanyonge bila aibu,”alisema Mbunge
huyo .
Alisema kuwa watendaji wa
serikari,DC na makada wa CCM pia ni viongozi wa kamati za ulinzi na
usalama katika maeneo yao ya kazi, hivyo wanapojiingiza
katika masuala ya aina hii umma wa Watanzania utakosa haki kwa kuwa
mmoja wa wahusika katika kuilinda haki hiyo atakuwa ameingia katika
mhimili hatarishi.
Mbunge huyo amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Muleba kufika
katika eneo la mgogoro huo ili kuutatua kuliko kutoa matamko akiwa ofisini
na kumuomba Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi,ambaye pia
ni Mbunge wa Jimbo la Muleba Kusini, Anna Tibaijuka alishughulikie suala
hilo.
Hata hivyo mbunge huyo ,alionyesha wasiwasi wake kuwa huenda hata Waziri huyo akashindwa kutatua
mgogoro huo kwa kuwa ni mmoja wa watuhumiwa wa uporaji wa ardhi, ambapo
yeye anadaiwa kuhodhi eneo linalokadiriwa kufikia ekari zaidi ya 1000
katika kijiji cha Kyamyorwa, huku yakiwepo madai ya mauaji ya watu wanne
wakati wa zoezi la kuwaondoa wananchi waliokuwa wanaishi katika eneo
linalodaiwa kumilikiwa na waziri huyo.
Aidha Viongozi hao wa CHADEMA wilayani humo, wamemuomba Rais Jakaya
Kikwete kufuta hati miliki tata za ardhi na zenye mashaka ili kuondoa
hali ya migogoro ya ardhi iliyoshamiri nchini na kusababisha mauaji
ya raia jambo linaloelezwa kuwa litaitumbukiza nchi kwenye machafuko.
Tanzania daima lilimtafuta
Mkuu wa Wilaya ya Muleba kupitia simu yake ya Mkononi namba 0767 008
888 simu yake iliita bila kupokelewa ndipo alipotumiwa ujumbe kutaka
ufafanuzi juu ya tuhuma hizo lakini hakuweza kujibu chochote.
Naye Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Muleba Muhaji Yusuf
Bushako,alipoulizwa kwa simu ya mkononi na gazeti hili kuhusu kuhusishwa
kwakwe kwenye utapeli wa ardhi inayolalamikiwa na Ushirika wa Wafugaji,
alidai hata yeye anausikia mgogoro huo na hahusiki kwa lolote.
Mbali na Mwenyekiti huyo wa CCM wa Wilaya ,mtuhumiwa
anayedaiwa kuwa msimamizi wa ardhi hiyo ya marehemu Barongo, Hamisi
Y Bilamata ,alipotafutwa kupitia simu zake za mkononi hazikuwa hewani
(0756 783 625 na 0789 522 180).
mwisho
![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEik0IHSmouWg-F9B-FCqXyQ0_-QWT7UkKqTzZKaRNmNGr1DTMO0uojDLoXKm_rM0UePPNcOuPB6VJ00lrW3KQWpTKRR9CSWxIgh6zUYafVU5bOFL6wP04fQIAXpd2XV3PbXqZc9cUAi-MA/s1600/unnamed1.jpg)
Dsc 00490 Diwani kata ya kasharunga akihutubia mamia ya wananchi waliohudhuria mkutano wa hadhara katika kijiji cha
kiteme
![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEi-63DfJ7C28nodnYZ8M6xHKRl_yF2_c02KP8iCLhrNMOdXqvgqnk23He84Xt2Oad0PcrMubMWt02OcPXvEPyZiQi9PahD0zOpUQ2Tq_Eg-tntzumI3OfjqMvkJBqQg8Z-IrWFUVm4E0_w/s1600/unnamed.jpg)
Mbunge wa Viti Maalum CHADEMA Conchester Mwamlaza akihutubia mamia ya
wananchi waliohudhuria mkutano wa hadhara katika kijiji cha kiteme
0 comments:
Post a Comment