Najitokeza katika ukurasa wako huu nitoe yangu ya
moyoni,hii ni kutokana na Taifa letu kuandamwa na migogoro ya Ardhi isiyokwisha.
Kwanza napenda kumpa pole,mzazi wa mtoto wa miaka 12
aliyefariki kwa kufyatuliwa risasi na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha
Mapinduzi na Diwani wa Kata ya Kisesa Clement Mabina na pili nawapa pole
Familia ya marehemu Clement Mabina,tatu nawapa pole viongozi wa Mkoa wa Mwanza
kwa kuondokewa na raia ambao kwa namna moja kila mmoja alikuwa akitegemewa na
familia yake na Taifa kwa mchango wake wa mawazo na mengine mengi.
Nikiwa nasoma shuleni mwalimu wangu wa kwanza kunifundisha
somo la Siasa ambaye ni Boniventura Shebo Nkuba aliwahi kutufundisha kuwa ili
Taifa lolote liweze kuendelea linahitaji vitu vine Ardhi, watu,Siasa safi na Uongozi
bora.
Nilijisikia amani kusikia hivyo na nilijifunza kuwa
kilichokuwa kikifundishwa endapo kingekuwa na ufuatiliwaji thabiti na wenye
mamlaka huenda kingeweza kuwa ni dira ya Taifa kama ilivyokuwa wakati wa Azimio
la Arusha.
Serikali ya Awamu ya kwanza hadi ya Nne tumeendelea kusikia
kauli hiyo lakini sasa,ufuatiliaji na utimilifu wa dira hii unaenda ukipotea
taratibu na watu wakiendelea kupoteza uvumilivu.
Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Jakaya Kikwete imekuwa ikipiga
kelele kuhusu kuondolewa urasimu katika umiliki wa Ardhi kwa wananchi kwanza na
baadaye kwa wawekezaji,katika sekta mbalimbali nchini,ikiwemo viwanda,biashara
na kilimo.
Cha kushangaza, watendaji wa Serikali wameshindwa kuwajibika
kwa wananchi walioiweka Serikali hiyo madarakani kuhusu kuwapatia Elimu juu ya
sheria ya Ardhi, tumeendelea kushuhudia madhara makubwa yanayoendelea
kulitafuna Taifa letu na watu wake.
Kila kukicha vilio,ugomvi kati ya wananchi wakulima na
wafugaji,wawekezaji na wananchi na hatimaye tunashuhudia Vigogo kujichukulia maeneno ya wananchi kwa kutoa
fedha kidogo nazo zikiishia mikononi mwa wajanja wachache wanaoongoza serikali
za vijiji au hakuna kabisa hata shilingi inayowasilishwa ili kuchangia
maendeleo katika maeneo husika.
Tunaona mfano kwa aliyekuwa mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi
na dunia wa Kata ya Kisesa jijini Mwanza marehemu Clement Mabina,kwa mujibu wa
mtoa taarifa Mgogoro kati ya wananchi na kigogo huyo unaonyesha kuwa haukuwa mpya, ulikuwa ni wa muda mrefu,
tunaona jinsi wananchi wanavyoweza kuwa na uvumilivu na hatimaye uvumilivu
ukiwashinda matokeo yake kuamua liwalo na liwe.
Kufuatia kushamiri kwa migogoro ya Ardhi hii Nchini ni
dalili tosha kuwa iwapo serikali haitachukua hatua za haraka huenda hali ikawa
mbaya zaidi.
Ninayo mifano mingi ya migogoro hiyo katika maeneo
mbalimbali nchini,wilayani kishapu kuna maeneo yaliyochukuliwa na mwekezaji na
wananchi mpaka leo wanalia na hakuna anaye wasikiliza kilio chao,Mpanda,Kibaha,
Nyamongo, Karagwe,Ngorongoro na maeneo mbalimbali Mkoani Morogoro,Mbeya,Dodoma
na maeneo mengine ipo migogoro
inayofukuta.
Ukisikiliza vyombo vya habari utasikia viongozi wakitoa
ahadi lukuki kuhusu kulinda maslahi ya taifa na huku wakisisitiza kuwa suala la
Ardhi ni nyeti na wananchi wapewe kipau mbele kwanza katika kumilikishwa Ardhi
kabla ya wageni.
Ukifuatilia kwa undani vigogo walio wengi pamoja na
matajiri wenye fedha zao wamejimilikisha maeneo makubwa huku wananchi wakiporwa
maeneo na wakipiga kelele kila kukicha bila mafanikio.
Kwa mfano Wilayani Muleba kuna
kigogo mmoja ambaye aliwahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera anayedaiwa kujipatia
ardhi yenye ukubwa wa ekari 8000 zaidi ya hekari alizoziomba, ambapo kigogo
huyo aliomba kupatiwa ekari 2000, uombaji ambao hata hivyo haukufuata kanuni na
taratibu, ikiwemo ushirikishwaji wa wananchi haukuzingatiwa,hivyo kuzua mgogoro
mkubwa.
Hivi kweli kwa hali hii tunaweza kukubaliana kuwa ili taifa
liendelee tunahitaji Ardhi,watu,siasa safi na uongozi bora?
Tanzania imebarikiwa kuwa na Ardhi tena iliyosheheni Madini
kama Almasi, dhahabu, Urani, gesi, mafuta, misitu,Wanyama, Mito, Maziwa, na
Bahari,rasrimali zote hizi zikiwa ni mali yetu sote.
Enzi za utawala wa Kanal Muamar Ghadaff wa Libya Watanzania
wote leo ,kila mmoja wetu angeingiziwa fedha
kwenye Akaunti yake ili aweze kunufaika na mali asili kutoka kwa Mungu
lakini si kwa nchi kama Tanzania kwa watu waliojenga imani ya Mimi kwanza
wengine baadaye kila mtu anavutia kwake.
Nina ushahidi kuwa Serikali pamoja na raia wake wote hakuna
mtu hata mmoja anayetozwa ushuru au kodi na mwenyezi Mungu kwa ajiri ya
maliasili hizi,vitu hivi vimepatikana bure kabisa.
Iweje leo tuhangaike Matibabu?
Iweje leo tuhangaike Ada za watoto wetu?
Iweje leo tuhangaike Madawa na majengo ya zahanati na hospitali?
Iweje leo kina mama wajawazito wajifungue kwa kununua
gloves na dawa za kuzuia damu wakati wa uzazi?
Je wapo viongozi tulio nao ni bora na wanaosimamia sera na
mipango ya serikali ili kuendeleza wananchi wake katika sekta za kilimo, Afya
na nyinginezo?
Je siasa zinazofanywa na wanasiasa wetu ni siasa safi kama
nilivyoanza kusema hapo awali?
Tunashuhudia viongozi wa ngazi za chini leo wanavyoifuga
migogoro hii kwa manufaa yao na kupelekea wananchi kujichukulia sheria mkononi,Mkoani
Morogoro na huko Ngorongoro wananchi wamjichukulia sheria mkononi huku wakivamia
vituo vya polisi kwa lengo la kuwakomboa wenzao na matokeo yake hali hiyo
ikapelekea mauaji ya raia kwa risasi za moto je hali hii ikiendelea kwa mfumo
wa kisiasa Taifa letu litakuwa mahali salama pa kukimbilia?.
Angalia wawekezaji wa migodi inayomilikiwa na kampuni ya Barrick kule Buzwagi jinsi walivyochukua maeneo huko Mwendakulima
na kuwaweka wananchi katika hali ngumu huku wakivuta vumbi lenye kemikali na huku
wakipiga kelele zao kwa viongozi bila mafanikio!
Hivi kweli iwapo wananchi watakapoingiwa na shetani wa
kukosa uvumilivu kama ilivyotokea kwa marehemu Clement Mabina Nchi yetu bado
itakuwa ni sehemu salama ya kuishi na kisiwa cha amani kama inavyojulikana
katika jumuia ya kimataifa!
Rai yangu kwa viongozi wa serikali pamoja na wananchi hebu
tuombe ibilisi huyo apishe mbali viongozi wa serikali nao watoe kipaumbele katika
kutoa Elimu ya uraia pamoja na sheria ya Ardhi kwa kushirikiana na makundi
mbalimbali zikiwemo asasi za kiraia ili kulinusuru taifa letu kuingia katika
migogoro mikubwa kati ya raia na Serikali,matajiri na maskini.
Mungu ibariki Tanzania!
Mwandishi wa makala hii ni mwanaharakati wa Haki za
Binadamu
0785 118118
0 comments:
Post a Comment