Na Antony Sollo na
Valence Robert Mwanza.
August 04.2014.
Mzani
Usagara ulioko Wilaya ya Misungwi jijini Mwanza unadaiwa kuchakachuliwa na
watumishi wa Wakala wa Barabara nchini TANROADS Tanzania Daima limebaini.
Wakizungumza na Tanzania Daima
baadhi ya Madereva wanaotumia Mzani huo kutoka Mikoa mbalimbali nchini wamelalamikia kitendo cha kupima katika Mizani
ya Mikoa mingine na Uzito wa Mizigo yao kuwa sahihi,lakini wanapofika katika
Mzani huo uzito wa Mizigo yao hubadilika na matokeo yake kuombwa rushwa na
wakikataa kutoa rushwa hupigwa faini kwa lengo la kukomolewa.
Madereva waliopatwa na mkasa
huo ni Khasim Hausi dereva wa Lori lenye namba za Usajili T 210 CAQ aina ya
Fusso.
Khasimu ameliambia Tanzania Daima kuwa wakati
anatoka Karagwe na kupima Mzani wa Kyaka mzigo wake ulikuwa na Kilo 6000 mbele
na upande wa nyuma ilikuwa ni kilo 9800 lakini alipofika Mzani wa Usagara Mzigo
wake ulipimwa na kuonyesha kuwa ulikuwa umezidi kilo 250 jambo ambalo hakukubaliana
nalo maana hakuongeza mzigo wa aina yoyote njiani.
Baada ya mtafaruku huo Dereva Khasim
aliambiwa atoe fedha kiasi ambacho ni kikubwa na kupelekea kuzua tafrani katika
eneo la mzani akilalamikia unyanyasaji wanaofanyiwa Madereva wanaotoka Mikoa mbalimbali
na watendaji wa Wakala wa Barabara TANROADS Mkoa wa Mwanza.
Tanzania Daima lilishuhudia
Dereva mwingine aliyepatwa na masahibu ya kuzidishiwa uzito kwenye gari
Photidas Kennedy ( 40 )mwenye gari namba T 864 CGD aina ya Fusso lililokamatwa
usiku wa terehe 02 August 2014 saa 4:00 usiku na kuombwa Rushwa ya shilingi
laki moja akidaiwa kuzidisha uzito ili aachiliwe aendelee na safari yake.
Kennedy alikataa kufanya hivyo,lakini
baada ya kusumbuliwa sana na mfanyakazi wa Mzani wa Usagara Yusuf Kasumla,Dereva
huyo alilazimika kutoa kiasi cha shilingi 75,000 na kuambiwa apange mzigo wake vizuri lakini
alipanga zaidi ya mara mbili bila mafanikio.
Tanzania Daima lilifika eneo
la Mzani na kulikuta gari T 864 CDG likiwa limepakiwa nje ya uzio wa TANROADS
ambapo alipouliza kulikoni alidokezwa kitendo cha kuombwa rushwa kwa Kennedy mfanyakazi
aliyemtaja kwa jina la Yusuf Kasumula.
Baada ya kufuatwa na waandishi
wa habari na kuhojiwa Kasumula alikiri kumfahamu Dereva huyo na kusema kuwa
gari hilo lilizidisha mzigo.
Kuhusu kulipa faini na kushindwa
kupewa risiti Kasumula alisema kuwa “taratibu za Ofisi ya TANROADS unalipa
kwanza na risiti utapewa baada ya mzigo wako kukaa vizuri.”
Tanzania Daima ilipata kuona
mkanganyiko katika risiti za malipo ambapo risiti ya tarehe 2 August 2014
inasomeka ni ya tarehe ya siku inayofuata.
Akizungumzia utata wa kusoma
tarehe ya siku inayofuata badala ya tarehe husika Mhandisi wa Tanroads Mkoa wa
Mwanza Pius Joseph aliliambia Tanzania Daima kuwa ni kweli kuna tatizo la
usomaji wa tarehe katika mzani huo.
“Ni kweli kuna tatizo la
kusoma kwa tarehe katika mzani huo tunalifahamu ni la muda
mrefu,tutalishughulikia.”alisema Joseph.
Kukiri kwa Mhandisi huyo juu
ya utata katika kusoma kwa tarehe kumethibitisha madai ya kuchakachuliwa kwa
Mzani wa Usagara.
Madereva mbalimbali wanaotumia
Mzani wa Usagara wameiomba Serikali ishughulikie tatizo hilo kabla
hawajatangaza mgogoro mkubwa ambapo walisema ifikapo Augosti 15 wataanza mgomo
utakaoendeshwa bila kikomo kwa kuweka magari kuzuia huduma ya Usafiri wa aina
yoyote kwa barabara ya Usagara Misungwi ,Kigongoferry na Sengerema.
Mwisho.
0 comments:
Post a Comment