Saturday, August 2, 2014

Kaimu Afisa Habari Misungwi afukuza Waandishi wa Habari kikao cha Baraza la Madiwani.

Mzani wa Usagara wadaiwa Kuchakachuliwa
Na Antony Sollo na Valence Robert Mwanza.
August 04.2014.

Mzani Usagara ulioko Wilaya ya Misungwi jijini Mwanza unadaiwa kuchakachuliwa na watumishi wa Wakala wa Barabara nchini TANROADS Tanzania Daima limebaini.


Wakizungumza na Tanzania Daima baadhi ya Madereva wanaotumia Mzani huo kutoka Mikoa mbalimbali nchini  wamelalamikia kitendo cha kupima katika Mizani ya Mikoa mingine na Uzito wa Mizigo yao kuwa sahihi,lakini wanapofika katika Mzani huo uzito wa Mizigo yao hubadilika na matokeo yake kuombwa rushwa na wakikataa kutoa rushwa hupigwa faini kwa lengo la kukomolewa.

Madereva waliopatwa na mkasa huo ni Khasim Hausi dereva wa Lori lenye namba za Usajili T 210 CAQ aina ya Fusso.

 Khasimu ameliambia Tanzania Daima kuwa wakati anatoka Karagwe na kupima Mzani wa Kyaka mzigo wake ulikuwa na Kilo 6000 mbele na upande wa nyuma ilikuwa ni kilo 9800 lakini alipofika Mzani wa Usagara Mzigo wake ulipimwa na kuonyesha kuwa ulikuwa umezidi kilo 250 jambo ambalo hakukubaliana nalo maana hakuongeza mzigo wa aina yoyote njiani.

Baada ya mtafaruku huo Dereva Khasim aliambiwa atoe fedha kiasi ambacho ni kikubwa na kupelekea kuzua tafrani katika eneo la mzani akilalamikia unyanyasaji wanaofanyiwa Madereva wanaotoka Mikoa mbalimbali na watendaji wa Wakala wa Barabara TANROADS Mkoa wa Mwanza. 

Tanzania Daima lilishuhudia Dereva mwingine aliyepatwa na masahibu ya kuzidishiwa uzito kwenye gari Photidas Kennedy ( 40 )mwenye gari namba T 864 CGD aina ya Fusso lililokamatwa usiku wa terehe 02 August 2014 saa 4:00 usiku na kuombwa Rushwa ya shilingi laki moja akidaiwa kuzidisha uzito ili aachiliwe aendelee na safari yake.

Kennedy alikataa kufanya hivyo,lakini baada ya kusumbuliwa sana na mfanyakazi wa Mzani wa Usagara Yusuf Kasumla,Dereva huyo alilazimika kutoa kiasi cha shilingi 75,000  na kuambiwa apange mzigo wake vizuri lakini alipanga zaidi ya mara mbili bila mafanikio.

Tanzania Daima lilifika eneo la Mzani na kulikuta gari T 864 CDG likiwa limepakiwa nje ya uzio wa TANROADS ambapo alipouliza kulikoni alidokezwa kitendo cha kuombwa rushwa kwa Kennedy mfanyakazi aliyemtaja kwa jina la Yusuf Kasumula.

Baada ya kufuatwa na waandishi wa habari na kuhojiwa Kasumula alikiri kumfahamu Dereva huyo na kusema kuwa gari hilo lilizidisha mzigo.

Kuhusu kulipa faini na kushindwa kupewa risiti Kasumula alisema kuwa “taratibu za Ofisi ya TANROADS unalipa kwanza na risiti utapewa baada ya mzigo wako kukaa vizuri.”

Tanzania Daima ilipata kuona mkanganyiko katika risiti za malipo ambapo risiti ya tarehe 2 August 2014 inasomeka ni ya tarehe ya siku inayofuata.

Akizungumzia utata wa kusoma tarehe ya siku inayofuata badala ya tarehe husika Mhandisi wa Tanroads Mkoa wa Mwanza Pius Joseph aliliambia Tanzania Daima kuwa ni kweli kuna tatizo la usomaji wa tarehe katika mzani huo.
“Ni kweli kuna tatizo la kusoma kwa tarehe katika mzani huo tunalifahamu ni la muda mrefu,tutalishughulikia.”alisema Joseph.

Kukiri kwa Mhandisi huyo juu ya utata katika kusoma kwa tarehe kumethibitisha madai ya kuchakachuliwa kwa Mzani wa Usagara.

Madereva mbalimbali wanaotumia Mzani wa Usagara wameiomba Serikali ishughulikie tatizo hilo kabla hawajatangaza mgogoro mkubwa ambapo walisema ifikapo Augosti 15 wataanza mgomo utakaoendeshwa bila kikomo kwa kuweka magari kuzuia huduma ya Usafiri wa aina yoyote kwa barabara ya Usagara Misungwi ,Kigongoferry na Sengerema.

Mwisho.





0 comments:

Post a Comment