Friday, August 1, 2014

Misungwi waomba Kuundwa kwa Wizara ya Wazee.


Misungwi  waomba Kuundwa kwa Wizara ya Wazee.


Na Antony Sollo  Mwanza.
June 18, 2014.

WAZEE Wilayani Misungwi wameitaka Serikali kuunda Wizara ya Wazee nchini,ili kuweza kusikiliza na kutekeleza sera ya huduma mbalimbali kwa wazee kama ilivyo katika kundi la Vijana  , kauli hiyo ilitolewa na washiriki wa semina iliyokuwa imeandaliwa na Tume ya kurekebisha Sheria iliyofanyika juni 17 katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi Mkoani Mwanza.

Ujio wa Tume hiyo Jijini Mwanza ni kwa ajili ya kufanya utafiti na kukusanya maoni juu ya mfumo bora wa sheria ya kusimamia huduma kwa wazee ambapo katika Mkoa wa Mwanza. Wilaya zilizokuwa katika mpango huo ni Wilaya ya Misungwi na Nyamagana.

Tume hiyo iliongozwa na Mwenyekiti wake Jaji Aloyce Mujulizi,akifuatana na wanasheria wa Tume hiyo Adamu Mambi,(Naibu Katibu),Bi Christina Binali (Mwanasheria Mwandamizi wa Tume ) na Japhet Daud ambaye pia ni  Mwanasheria wa Tume hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari Wilayani Misungwi,Jaji Mujulizi alisema kuwa Tume hiyo ilianzishwa chini ya kifungu cha 3 cha sheria ya kurekebisha sheria  namba 11 ya mwaka 1980,ambpo sheria hii kwa sasa ni sura ya 171 ya sheria za Tanzania toleo la mwaka 2002.

Jaji Mujulizi alisema kuwa Tume hiyo ni Idara ya Serikali inayojitegemea chini ya Wizara ya Katiba na sheria ambapo Tume hii ilianza kufanya kazi rasmi 21 Oktoba 1983 na kwamba tangu kuanzishwa kwake zaidi ya taarifa thelathini  (30) zenye mapendekezo zimewasilishwa Serikalini na tayari sheria mbalimbali zimefanyiwa marekebisho kutokana na mapendekezo ya Tume hiyo.

Jaji Mujulizi ameyataja majukumu ya tume hiyo kuwa ni kufanyia mapitio sheria zote za Tanzania na kutoa mapendekezo ya marekebisho ,kwa kutathmini maeneo yote ya sheria husika na kuyatolea mapendekezo kwa lengo la kuyaboresha,na baada ya utafiti huo tume inapeleka ripoti  kwa Waziri wa sheria na Katiba kwa hatua zinazofuata.

Akiendelea kutoa ufafanuzi kuhusu majukumu ya Tume hiyo,Jaji Mujulizi alisema kuwa,mapendekezo ya Tume hiyo yamekuwa yakitiliwa maanani na serikali wakati wa kutunga sheria na kanuni na kwamba serikali imekuwa ikitoa miongozo ya kiutawala kutokana na mapendekezo ya Tume ili kuondoa kasoro zilizoainishwa na wadau pamoja na Tume.

Katika mada iliyotolewa juu ya utoaji huduma kwa wazee nchini Tanzania Elderly Social Care in Tanzania,umri wa kustaafu kwa mujibu wa sheria ni miaka 60,lakini iko wazi kwamba sio watu wote wenye umri huo na zaidi hawana nguvu za kufanya kazi wakati huohuo baadhi ya watu wenye umri chini ya miaka 60 wanakuwa hawana uwezo au nguvu za kufanya   kazi.

Kwa mujibu wa Mujulizi inakadiriwa kuwa zaidi ya watu milioni 1.4 wana umri wa miaka 60 na zaidi,na inakadiliwa kuwa ifikapo mwaka 2050 idadi itaongezeka na kufikia watu milioni 8 kwa mujibu wa taarifa ya kabla ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2002 na taarifa ya maendeleo Tanzania,mapitio ya MIPAA,katika kikao kilichokaa Addis Ababa Ethiopia tarehe 19-21 Novemba 2007.
Jaji Mujulizi alisema kuwa idadi kubwa ya wazee Tanzania wako kwenye matatizo makubwa kwa sababu ya kutopata huduma na ulinzi mzuri Social and Security Servises kwa kuwa wazee walioko kwenye mfumo rasmi ni wale walioko kwenye ajira pekee,ambao hupata huduma katika mifuko ya jamii kama vile NSSF,PPF,PSPF,NHIF,LAPF,GEPF ambapo mifuko hii hutunza akiba za wafanyakazi ( pensheni ) ambapo huwalipa baada ya kustaafu.

Kufuatana na hali hiyo,Tume ya kurekebisha sheria nchini imeamua kufanya utafiti katika eneo hili ili kubaini mapungufu yaliyopo kuhusiana na mfumo mzima wa utoaji huduma kwa wazee Tanzania,kupitia mapungufu yake ili kufanyiwa maboresho na katika hali hii Tume inakaribisha wadau mbalimbali kutoa maoni yao katika kufanikisha zoezi hili alisema Jaji Mujulizi.

Wakichangia mada hiyo,wazee hao walitoa mapendekezo mbalimbali ikiwemo kuwepo kwa dirisha la huduma kwa wazee katika Halmashauri za Wilaya nchini ,kuundwa kwa taasisi maalumu zinazotoa huduma kwa wazee, Benki,vyombo vya usafiri, nk ili kuwaondolea usumbufu wazee nchini.

Mwisho.

0 comments:

Post a Comment