Thursday, June 26, 2014

Wizi wa Mafuta Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi

Wizi wa Mafuta Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi


  • Dereva adaiwa kugushi nyaraka na kuiba mafuta.

  • Aandika vibali feki kwa magari manne lita 270.

Dereva mmoja wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi  jina tunalo,anatuhumiwa kutengeneza nyaraka kwa ajili ya kuchukua mafuta ya magari manne kwa lengo la kuiibia Halmashauri.

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi umebaini kuwa wizi huo ulifanyika kati ya tarehe 01/06/2014 na tarehe 5/06/2014 ambapo tarehe juni 01 haikuwa siku ya kazi na wala hakukuwa na dharula yoyote iliyotokea kwa mujibu wa chanzo cha habari hii.

Imeelezwa kuwa Dereva wa Lori namba SM 3283 alitengeneza vibali feki vya mafuta ya magari manne kwa Invoice namba 000316 ya juni 01 mwaka huu toka idara ya Afya akiomba kupatiwa mafuta aina ya Diesel kiasi cha lita 60 kwa ajili ya kwenda kusambaza chanjo vijijini kwa kutumia gari namba STJ 2505.

Kwa mujibu  wa mtoa taarifa imeelezwa kuwa Dereva huyo alikwenda kituo cha mafuta cha Smat Usagara na kupewa mafuta hayo huku akiwa amegushi sahihi ya dereva mwenzie J. malimi kwa mujibu wa nyaraka hiyo.

Siku ya tarehe 05 juni mwaka huu mtuhumiwa huyo alitengeneza vibali vya magari matatu kwa kutumia invoice namba 001890 toka idara hiyohiyo ya Afya akiomba mafuta aina ya diesel kiasi cha lita 210 kwa kuyapangia kazi kama ifuatavyo, STJ 1189 lita 90 kwa ajili ya dharula ya wagonjwa, gari ambalo liko kituo cha Afya Mbalika Wilayani Misungwi huku akighushi sahihi ya dereva wa gari hilo Benjamini Bukindu. 
Magari mengine ni SM 4774 lita 70 kwa ajili ya shughuli za utawala,gari hili likielezwa kuwa dereva wake Makoye Mwilima alikuwa mgonjwa kwa muda wa  mwezi mzima na gari lake lilikuwa limepaki.

Gari lingine ni STJ 4505 lita 50 kwa ajili ya shughuli ya kusambaza chanjo vijijini gari ambalo haliko katika orodha ya magari ya Halmashauri ya Wilaya hiyo.
Akiongea na Tanzania Daima kwa sharti la kutoandikwa jina lake gazetini,dereva wa gari mojawapo linaloonekana lilichukuliwa kibali cha kwenda kuchukua mafuta hayo amesema nimesikitishwa sana na tukio hili kwakuwa linajenga hisia mbaya kwa utumishi na ninaomba vyombo vya dola vichukue hatua kwa mhusika kwa vile alikuwa na nia mbaya na sisi

Mwandishi wa Habari hizi alimtafuta Dereva huyo kutaka kupata ufafanuzi wa tuhuma zilizotolewa dhidi yake kwa namba za simu ya mkononi namba ­0759123924 ambapo alisema yuko Mkoani geita akiuguza mgonjwa na kusema kuwa “ndugu mwandishi mimi niko Geita nauguza mgonjwa na gari langu liko kijijini linasomba mchanga na mimi sipo Misungwi”

Mkurugenzi wa Wilaya ya Misungwi Nathan Mshana amekiri kuwepo kwa tukio hilo na kusema kuwa baada ya kupata taarifa hizo anazifanyia uchunguzi na mhusika akibainika na kosa hilo atachukuliwa hatua za kisheria kwa kupelekwa kwenye vyombo vya sheria ili sheria ichuke mkondo wake.

Mwisho

0 comments:

Post a Comment