Friday, January 30, 2015

Wafugaji waichanganya Serkali.



Wafugaji waichanganya  Serkali.
Na Antony Sollo.

CHAMA cha Wafugaji Nchini CCWT kimeichanganya Serikali baada ya kuibuka kuwa makundi mawili yanayohasimiana na kusababisha mgororo mkubwa ndani ya chama hicho.
Hayo yalibainishwa juzi na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Dk Titus Kamani wakati wa mkutano wake na waandishi wa Habari uliofanyika Ofisini kwake mjini Dodoma.

Dk kamani aliiwaambia waandishi wa habari lengo la mkutano huo lilikuwa ni kutolea ufafanuzi juu ya mambo mawili
,mgogoro kati ya wakulima na wafugaji uliotokea Mkoani Morogoro pamoja na mgogoro unaofukuta ndani ya chama cha Wafugaji Nchini CCWT.

Akitoa ufafanuzi huo kwa waandishi wa Habari Dk  Kamani alisema kuwa chama hiki kimesababisha usumbufu mkubwa kwa wafugaji baada ya kuanzisha malumbano kati ya pande zote mbili jambo linalowafanya wakose msimamo na imani na chama ambacho kilianzishwa kwa lengo la kuwakomboa wafugaji hao.

Kuhusu kushamiri kwa matumizi ya risasi kwa makundi ya wakulima na wafugaji wakati wa migogoro katika maeneo mbalimbali nchini Dk Kamani alisema kuwa kumpiga mtu risasi ni kosa na huu ni uhalifu kama uhalifu mwingine hivyo alionya kuwa wote watakaobainika kufanya vitendo hivyo watachukuliwa hatua za kisheria.

Waandishi wa Habari walipotaka kujua ni nini msimamo wa Dk Kamani kuhusu  mwaliko wa Jan 30 Dk Kamani alisema kuwa hayuko tayari kuhudhuria Mkutano wowote wa chama hicho mpaka pale watakapolipatia ufumbuzi suala hilo ili Kundi hilo liweze kupata uhalali wa kutumia nembo na jina la Chama cha Wafugaji Taanzania CCWT.

 Hata hivyo Mwenyekiti wa chama cha Wafugaji Nchini  CCWT  taifa  Ally Lumiye alikiri kuwepo kwa makundi ndani ya chama hicho .
“ ni kweli kuna makundi ndani ya CCWT  kuna kiongozi ambaye yuko katika kundi la pili, huyu ni aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCWT George Kifuko ambaye alifukuzwa na baadaye alifadhiliwa na wakala aliyepewa tenda na Wizara ya Mifugo kwa ajili ya kusambaza madawa ya ruzuku,Gresso Bajuta ili kuchochea vurugu ndani ya Chama cha Wafugaji ”.alisema Lumiye.

Akifafanua Lumiye alisema kuwa kabla ya kuibuka kwa mgogoro huo,Bajuta alikuwa mjumbe wa bodi ya wadhamini wa chama cha Wafugaji na kubainisha kuwa wakati chama kinamteua kuwa mjumbe wa bodi hiyo hawakujua kama Bajuta alikuwa ndiye mmiliki wa Kampuni ya Bajuta International na ambayo ilipewa tenda na Serikali kwa ajili ya kusambaza madawa ya ruzuku.

Imefahamika kuwa baada ya kufanya ziara nchi nzima, Mwenyekiti wa CCWT Ally Lumiye alipata malalamiko toka kwa wafugaji kwamba hawapati madawa ya ruzuku kabisa, baada ya ufuatiliaji  ilibainika kuwa aliyekuwa amepewa tenda ya kusambaza madawa hayo ni Bajuta International.

Kwa mujibu wa  sheria ya manunuzi PPRA hali hiyo ilipelekea ,mmiliki wa kampuni ya Bajuta International Gresso Bajuta kukosa sifa ya kuwa mjumbe wa bodi ya wadhamini kutokana na mgongano wa kimaslahi ya moja kwa moja.

Imeelezwa kuwa baada ya mtafaruku huo Gresso  alianza kumfadhili aliyekuwa katibu Mkuu wa CCW T George Kifuko  kwa lengo la kuchochea mgogoro na mgawanyiko ndani Chama hicho.

Kufuatia kufanyika kwa Mkutano Mkuu wa CCWT Ally  alisema kuwa Mkutano uliofanyika ukumbi wa IRDP tarehe 24/25 mwaka huu ni halali na kwamba Mkutano huo  ulitoa tamko la kuiomba serikali iingilie kati mgogoro unaosababishwa na wakala anayelalamikiwa kutofikisha madawa ya ruzuku kwa wafugaji.

Mkutano huo ulihudhuriwa na wanachama toka wilaya 17 zilizowakiliswa na wajumbe 4  pamoja na wafugaji 120 kutoka nchi nzima walihudhuria huku Ally akizitaja Wilaya zilizoshinikizwa kutoshiriki mkutano huo kuwa ni Bariadi,Meatu,Igunga na Mkarama.

Tanzania Daima lilimtafuta Wakala wa Madawa ya ruzuku ambaye ndiye mmiliki wa Kampuni ya Bajuta Inernational, Gresso Bajuta ili kutoa ufafanuzi juu ya tuhuma za kuchochea mgawanyiko ndani ya CCWT ambapo  alijibu kwa mkato kuwa yeye hana la kuzungumza.

“Mimi sina la kuzungumza maana mimi si msemaji wa CCWT mimi ni mjumbe wa bodi ya wadhamini wa muda,lakini pia mimi ni mfugaji tu hivyo kwa haya unayoniuliza sina la kusema”.alisema Gresso.

Mwisho.
 

0 comments:

Post a Comment