Waliopigwa risasi na
Askari wa Mgodi wailalamikia Serikali.
Na Antony Sollo,
Kishapu.
WANANCHI wa kijiji cha Maganzo na vitongoji
vyake wameilalamikia Serikali kwa kushindwa kusikiliza kero na adha wanayoipata
kutoka kwa Mwekezaji wa mgodi wa WDL kufuatia mashambulizi ya mara kwa mara
yanayofanywa na Askari wa Mgodi huo
Jilala Miligwa
ameliambia Tanzania Daima kuwa amechukua hatua ya kufikisha kilio hicho kwa
Rais Jakaya Kikwete akimuomba aingilie kati suala hili baada ya yeye na wenzake
tisa kujeruhiwa mgodini hapo huku kukiwa hakuna juhudi zozote zinazofanyika ili
waweze kulipwa fidia kutokana kushambuliwa kwa risasi za moto na askari wa
mgodi huo.
Akizungumza kwa niaba
ya wenzake wanane Jilala alisema kuwa ameamua kupeleka malalamiko hayo kwa Rais
Kikwete kutokana na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Sospeter Muhongo
kushindwa kulitafutia ufumbuzi suala hilo akiwa katika ziara yake Jan 8 Mkoani
Shinyanga.
Katika ziara hiyo Muhongo alipokuwa
akiongozana na Mbunge wa Jimbo la Kishapu Suleman Nchambi na kupatiwa taarifa
za kujeruhiwa kwa vijana hao aliahidi kutatua tatizo lao mapema kwa kuuagiza
uongozi wa mgodi kuwalipa fidia.
“Ndugu zangu naomba niwahakikishie,Serikali
yenu iko tayari kuwasikiliza na kutatua matatizo yenu hivyo kuanzia sasa
naagiza uongozi wa Mgodi wa Mwadui uwalipe fidia haraka iwezekanavyo” alisema
Muhongo.
Jilala ameliambia Tanzania Daima kuwa Muhongo pamoja na
Mbunge waliwaahidi vijana hao kuwa wangekutana na Uongozi wa Mgodi januari 19
mwaka huu lakini cha kushangaza si Mbunge wala Waziri aliyefika kwa lengo la
kutekeleza ahadi hiyo.
Jilala alilalamikia tabia ya Mbunge
huyo kutoa ahadi ambazo mara kadhaa hazitekelezeki na anapoulizwa anajibu
kisiasa jambo ambalo linawakera wananchi hao.
“Nchambi amekuwa na tabia ya
kutumia matatizo yetu kujizolea umaarufu ndani ya Bunge na kwenye majukwaa ya
siasa akitumia maneno matamu ambayo yanafanana na ukweli lakini utekelezaji
wake ni hovyo…alisema Miligwa.
“Mbunge wetu amekuwa akituahidi kuwa
atatusaidia kupata fidia bila mafanikio,tumeona kuwa anapenda kujipendekeza kwa
viongozi wa kitaifa pindi wanapokuwa na ziara Mkoani hapa.
Akichangia katika vikao vya
Bunge Nchambi amekuwa hodari wa kutoa kauli na kujigamba kuwa yupo tayari kufa
kwa ajili ya wanyonge ambao wanapoteza haki zao lakini anachokisema ni
tofauti na anachokitenda” alisema Miligwa.
Kabla ya kujiuzuru Tanzania Daima
lilimtafuta aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini,Sospeter Muhongo ili aweze
kutoa ufafanuzi wa malalamiko hayo lakini hakuweza kupokea simu kwa wakati.
Baada
ya kusumbuliwa kwa kuandikiwa ujumbe mfupi wa simu ya mkononi ndipo
alipofunguka na kuweza kujibu japo hakuweza kutoa ufafanuzi juu ya ufumbuzi wa
vijana hao kupitia Wizara Nishati.
Ujumbe mfupi wa Waziri ulikuwa hivi”
“Huo ni uzushi! Mimi niliagiza uchunguzi ufanyike wa wale wote wanaolalamika!
Utalipa bila kuchunguza?utalipa bila kufuata sheria na kanuni zake?” kwa nini
vijana hawa wanaogopa kwenda Mahakamani kwenye haki? Kwa nini hawafungui kesi
Mahakamani? Waende Mahakamani “alihoji Prof Muhongo.
Tanzania Daima lilipotaka kujua ni
hatua gani zitafuata baada ya uchunguzi huo kukamilika ,Waziri Muhongo alisema
kuwa ni vyema kuwa waangalifu,kama kweli unaonewa au umedhulumiwa hakuna sababu
ya kusita kwenda Mahakamani Wizara itasaidia lakini kila upande unayo haki ya
kwenda Mahakamani.
Kuhusu
ahadi ya Serikali kuwasaidia vijana hao Muhongo alisema kuwa baada ya uchunguzi
huo atahakikisha Haki inatendeka pande zote zinazohusika,kama hawatakubaliana
na kikao kitakachosimamiwa na Wizara basi itabidi waende Mahakamani.
“ili uweze kuupata ukweli ni lazima
usikilize pande zote mbili,uamzi hauwezi kutolewa kwa kusikiliza upande mmoja”
alisisitiza Muhongo.
Mbunge
wa Jimbo la Kishapu alipopigiwa simu 0767 444 148 ili kutolea ufafanuzi juu ya
malalamiko ya wananachi hao alikata simu na hata alipopelekewa ujumbe
akiombwa kutolea ufafanuzi juu ya malalamiko hayo alijibu kwa meseji fupi
“Siyajui”
Mwisho.
0 comments:
Post a Comment