Ni kwa tuhuma za kuomba na kupokea Rushwa
Na Antony Sollo Mwanza.
August 5.2014.
MFANYAKAZI
wa Mzani wa Usagara Jijini Mwanza,Yusuf Kasumula amehojiwa kwa zaidi ya saa
saba na Maafisa wa Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa TAKUKURU,akituhumiwa
kuomba na kupokea Rushwa akiwa kazini imefahamika.
Tukio
hilo lilitokea August 2 mwaka huu majira ya saa 4 : 00 Asubuhi katika eneo la
Usagara Mzani wa Usagara baada ya Photidas Kennedy ( 40 ) Dereva wa gari namba za
usajili T 864 CGD aina ya Fusso lililokamatwa usiku wa terehe 02 August 2014
saa 4:00 usiku na kuombwa Rushwa ya shilingi laki moja,akidaiwa kuzidisha uzito
wa mzigo katika gari lake.
Imedaiwa
kuwa mtumishi wa Mzani wa Usagara Yusuf Kasumula aliomba kiasi hicho cha fedha ili
amuachilie Kennedy aendelee na safari yake jambo ambalo Kennedy alilipinga
vikali.
Baada ya kusumbuliwa muda
mrefu Kennedy alilazimika kutoa kiasi hicho cha fedha shilingi 75,000 na kumpa Kasumula na baada ya hapo Kennedy aliomba
msaada kwa Maofisa wa Takukuru.
Tukio hilo liliripotiwa kwa
mwandishi wa habari wa gazeti hili ambaye alishirikiana na Kennedy kutafuta
ufumbuzi wa tukio hilo ambapo kwa pamoja walitoa taarifa kwa Kaimu Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Mwanza Christopher Cyprian Foime ambaye aliwasiliana na Uongozi wa Taasisi ya
kuzuia na kupambana na rushwa Mkoa wa Mwanza.
Kamanda wa Takukuru Mkoa Mwanza
aliwajulisha Maafisa wa Taasisi hiyo Wilaya ya Misungwi Julian Augustine wakiwa
na Dereva Bahati Nzumbi walifika Usagara na kufanya mahojiano na Yusuf Kasumula.
Wakizungumza na Tanzania Daima baadhi
ya Madereva wanaotumia Mzani huo kutoka Mikoa mbalimbali nchini ,wamelalamikia
kitendo cha kupima katika Mizani ya Mikoa mingine na Uzito wa Mizigo yao kuwa
sahihi,lakini wanapofika katika Mzani huo uzito wa Mizigo yao hubadilika na
matokeo yake kuombwa rushwa na wakikataa kutoa rushwa hupigwa faini kwa lengo
la kukomolewa.
Madereva waliopatwa na mkasa huo ni
Khasim Hausi dereva wa Lori lenye namba za Usajili T 210 CAQ aina ya Fusso.
Khasimu ameliambia Tanzania Daima kuwa wakati
anatoka Karagwe na kupima Mzani wa Kyaka mzigo wake ulikuwa na Kilo 6000 mbele
na upande wa nyuma ilikuwa ni kilo 9800.
Khasim amedai kuwa
alipofika Mzani wa Usagara Mzigo wake ulipimwa na kuonyesha kuwa ulikuwa
umezidi kilo 250 jambo ambalo hakukubaliana nalo maana hakuongeza mzigo wa aina
yoyote njiani.
Baadaye Khasim
aliombwa
atoe fedha kiasi ambacho ni kikubwa na akalalamikia
unyanyasaji wanaofanyiwa Madereva wanaotoka Mikoa mbalimbali nchini
na
watendaji wa Wakala wa Barabara TANROADS Mkoa wa Mwanza.
Baada ya kufuatwa na waandishi wa
habari na kuhojiwa kuhusiana na madai ya Khasim na Kennedy Kasumula
alikiri kuwafahamu Madereva hao na
kusema kuwa Magari yao yalizidisha
uzito.
Kuhusu kulipa faini na kushindwa kupewa
risiti Kasumula alisema kuwa “taratibu za Ofisi ya TANROADS unalipa kwanza na
risiti utapewa baada ya mzigo wako kukaa vizuri.”
Katika kile kinachodaiwa
kuwatisha Maafisa wa Takukuru,mzani wa Usagara unasoma nyaraka zake tofauti na
sehemu zingine kwa kuwa iwapo utapima mzigo wako hapo tarehe 5 August mwaka huu
nyaraka zako zitaonyesha ulipima tarehe 6 August jambo ambalo madereva na wadau
mbalimbali wamedai kuwa iwapo kuna makosa katika usomaji wa tarehe basi kuna
mashaka makubwa hata katika upimaji wa uzito wa mizigo.
Uchunguzi
uliofanywa na Tanzania Daima umebaini kuwa,kuna dalili za wizi na ubadhilifu
mkubwa unaofanyika katika Mzani wa Usagara kwani hata usomaji wa nyaraka katika
mzani huo hauendani na uhalisia.
Akizungumzia utata wa kusoma tarehe ya
siku inayofuata badala ya tarehe husika Mhandisi wa Tanroads Mkoa wa Mwanza
Pius Joseph aliliambia Tanzania Daima kuwa ni kweli kuna tatizo la usomaji wa
tarehe katika mzani huo.
“Ni kweli kuna tatizo la kusoma kwa
tarehe katika mzani huo tunalifahamu ni la muda
mrefu,tutalishughulikia.”alisema Joseph.
Kukiri kwa Mhandisi huyo juu ya utata
katika kusoma kwa tarehe kumethibitisha madai ya kuchakachuliwa kwa Mzani wa
Usagara.
Wakizungumzia kwa uchungu
dhidi ya uonevu wanaofanyiwa na watendaji wa Mzani wa Usagara Madereva
mbalimbali wanaotumia Mzani wa Usagara wameiomba Serikali ishughulikie tatizo
hilo kabla hawajatangaza mgogoro mkubwa ambapo walisema ifikapo Augosti 15
wataanza mgomo utakaoendeshwa bila kikomo kwa kuweka magari kuzuia huduma ya
Usafiri wa aina yoyote kwa barabara ya Usagara Misungwi ,Kigongoferry na
Sengerema.
Maafisa hao wa Takukuru walichukua takribani
masaa saba kuchukua maelezo ya na Yusuf na baada ya mahojiano hayo,waliondoka na
nyaraka mbalimbali zinazotumika katika Mzani uo kwa uchunguzi.
Mwisho.
0 comments:
Post a Comment